KUSHOTO: Rimsha akitoroshwa kwenye helikopta. KULIA: Rimsha akipelekwa kupanda helikopta. |
Msichana wa Kikristo ambaye
alituhumiwa kimakosa kwa kumkashifu Mungu nchini Pakistan, amepata
bandari salama na familia yake nchini Canada.
Agosti mwaka jana, inadaiwa Rimsha Masih mwenye miaka 14 alishitakiwa kwa kumkashifu
Mungu baada ya jirani mmoja kuripoti kumwona binti huyo akichoma kurasa
za Kitabu Kitakatifu cha Kur'an.Kosa kama hilo hukumu yake ni kifo nchini Pakistan, ambayo inaimarisha sheria zake za kidini wakati wa kipindi cha ukale katika miaka ya 1980.
Japo Rimsha hatimaye alifutiwa mashitaka, familia yake bado haikuwa salama kuishi nchini Pakistan.
Mara kwa mara ilipokea vitisho na hakika ikalazimika kuondoka.
Machi 14, mwaka huu Rimsha alihamia nchini Canada na wazazi wake, dada zake watatu, na kaka yake, kwa mujibu wa mwanasheria Tahir Mehmood Ashrafi.
Walifanikisha kuhama kwa msaada wa Shirika moja la Kikristo, na sasa wanaishi mahali fulani katika eneo la Toronto.
Peter Bhatti, ambaye anaongoza shirika hilo lililoisaidia familia ya Masih alieleza kwamba Rimsha 'anaendelea vema' na anahudhuria shule kila siku.
Ndoto hiyo ya binti huyo ilianza Agosti mwaka jana pale jirani Muislamu mshika dini kuripoti kwamba alimwona msichana huyo akichoma kurasa za Kur'an karibu na nyumbani kwao huko Mehrabadi jirani na mji wa Islamabad.
Tuhuma hizo zilivutia kundi la watu kati ya 500-600 kukusanyika nje ya nyumba ya Rimsha, na kuitolea vitisho familia hiyo ya Kikristo.
"Watu wengi walikusanyika na walikuwa wakisema: "Tutaikata mikono ya watu waliochoma Kur'an," dada wa Rimsha alieleza.
Rimsha alijifungia bafuni na hakutoka nje hadi polisi walipowasili na kumkamata. Binti huyo alikaa jela kwa siku 25.
Ingawa tuhuma hizo zilisababisha ghasia jirani na kwao, kulikuwa na wengi nchini Pakistan ambao walikuwa wakimpigania afutiwe mashitaka.
Mmoja wa kiongozi mwenye msimamo mkali wa kidini, Ahmed Ludhianvi, alisema kesi hiyo inatakiwa kuchunguzwa kwa umakini hasa kwa kuzingatia kwamba 'Uislamu hauruhusu yeyote kuhukumiwa papo hapo."
Hatimaye aliyemtuhumu aligundulika kuwa na ushahidi wa kughushi, na Rimsha akafutiwa mashitaka.
Lakini hukumu ya sheria sio sawa na hukumu ya umma, na familia ya Rimsha ikaendelea kuishi kwa hofu ndani ya nchi yao.
"Nina huzuni kwamba binti huyu asiye na hatia alilazimika kuondoka nchini Pakistan. Alikuwa amefutiwa mashitaka na mahakama, na licha kwamba hakukuwa na uwezekano wa yeye kuishi kwa uhuru,"Ashrafi alieleza
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni