Vilio na simanzi vilitanda Jumatano iliyopita Mwananyamala Kisiwani, jijini Dar kufuatia mtoto wa mwaka mmoja, Rahim Rajab kufariki dunia kwa kuangukiwa na watu watatu, akiwemo baba yake mzazi, Rajab Said..
Tukio la watu hao
kumwangukia mtoto huyo lilitokea Jumatatu iliyopita na lilisababishwa na
ugomvi mkubwa wa CD yenye nyimbo za mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu
Abdul ‘Diamond’ ulioibuka ndani ya chumba cha kulala kati ya mama wa
marehemu na mpangaji mwenzake aitwaye Aisha.
Akizungumza
kwa machungu kuelezea tukio hilo, mama mzazi wa marehemu Rahim, Habiba
Ally alikiri kuwa kisa cha kifo cha mwanaye ni CD tu.Akasema:
"Kwa kweli hakuna kingine zaidi ya CD, naamini hivyo kwa kuwa mimi
sikuwa na ugomvi wowote na Aisha. Tulikuwa tunaishi kawaida tu ukiacha
mikwaruzo ya hapa na pale.”
Akaongeza: Jumamosi iliyopita,
Aisha alikuja ndani kwangu na CD zake tatu, ya Diamond, Kingwendu na ya
Coast Modern Taarab. Alipomaliza kuangalia aliziacha, akaondoka zake.
“Jumapili mimi nikaenda nazo kwa mama zote tatu kwa ajili ya kuziangalia, tulipomaliza na mimi niliziacha huko.
“Jumatatu usiku Aisha akaja kunidai, nikamwambia zipo kwa mama. Kwa kuwa anapajua anapoishi mama, si mbali akaenda kuzichukua zote tatu.
Ajabu aliporudi
tu, akaja tena kwangu na kusema hajapewa CD ya Diamond kitu ambacho si
kweli na ndipo ulipozuka ugomvi wote huo hadi kusababisha kifo cha
mwanangu.”
Akizungumza msibani juzi, bibi wa marehemu, Jamima Hassan
alisema siku ya tukio alipigiwa simu na mkwe wake (baba wa marehemu)
akamwambia kuna ugomvi nyumbani kwake unaohusu CD kati ya mkewe na
mpangaji mwenzake ambapo bibi huyo aliamua kwenda kutatua ugomvi huo.
“Niliondoka muda huohuo kwani huyo Aisha alitoka kwangu kuchukua CD zake muda mfupi tu, sasa nilijiuliza ni CD gani wanazogombania?
“Nilipofika
nilikuta ugomvi umepamba moto, baba wa mtoto na mume wa Aisha aitwaye
Shaban Sangali walikuwa wameungana kumtoa nje ya chumba Aisha bila
mafanikio.
“Wakati naingia, Aisha alikuwa akitukana matusi mazito na tulipojitahidi kumtoa nje alitusukuma kwa nguvu. Ndipo yeye, mume wake na baba wa mtoto waliwaangukia watoto waliokuwa wamelala kitandani,” alisema bibi huyo.
Akaendelea: Tulipowaangalia watoto ambao ni mapacha, hali zao zilikuwa mbaya, tukaamua kwenda kwa mjumbe wa mtaa kuripoti, akatupa barua, tukaenda Kituo cha Polisi Mwinyijuma, pale wakatupa PF3 ya kuwapeleka Hospitali ya Mwananyamala ambako walilazwa kwa matibabu.
Bibi huyo alisema siku iliyofuata, Rahim alifariki dunia, ikabidi waende Polisi Oysterbay ambapo walifungua shitaka lenye faili kwa kumbukumbu No. OB/RB/1150/2013 MAUAJI.
Watuhumiwa katika RB hiyo ni Aisha na mumewe, Sangali ambao walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi.
Majirani
waliozungumza na mwandishi wetu walisema wakati ugomvi kati ya Aisha na
Habiba unatookea, mume wa Habiba alikuwa anarudi kutoka kazini,
akakutana na kimbembe hicho.
Walisema aliingilia kati kuamua
bila mafanikio. Wakati huo mume wa Aisha alikuwa chumbani kwake na
amefungulia muziki wa redio kwa sauti ya juu hivyo hakujua nini
kinaendelea kwenye chumba cha mpangaji mwenzake.
Ikaelezwa kuwa, kuna watu walikwenda kumgongea na kumwambia mkewe anapigwa na mume wa Habiba kwa kushirikiana na mkewe.
Ilibidi
mwanaume huyo atoke mbio hadi chumbani kwenye ugomvi ambako alikuta
baba wa marehemu akijitahidi kuwaamulia wawili hao bila mafanikio.
Habari zinasema mwanaume huyo aliingilia kati kuongeza nguvu lakini katika hali ya kuwalemea, Aisha aliwasukuma wote na kisha wao kuwaangukia watoto hao mapacha waliokuwa wamelala kwenye kitanda kimoja.
Katika hali ya kusikitisha, marehemu amemuacha pacha mwenzake aitwaye Rahima Rajab ambaye ni kulwa.
Wengi
wanaamini kuwa maisha ya Rahima yangekuwa ya furaha zaidi kama Rahimu
angekuwepo na kwamba itamsononesha sana akikua na kusikia mwenzake
alifariki dunia kwa ugomvi wa mama yake na mpangaji mwenzao kisa ni CD
ya nyimbo za mwanamuziki.
GPL
GPL
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni